The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050: Wafanyakazi Wanapokosa Nguvu, ni Ngumu kwa Mwananchi Kunufaika na Ukuaji wa Uchumi

Tukuze uchumi ndiyo, lakini tuhakikishe ukuaji huo hautokei katika namna inayoathiri maslahi ya watu walewale ambao nguvu na jasho lao ndiyo zinategemewa kujenga nchi.

subscribe to our newsletter!

Mtazamo wangu binafsi ni kwamba, kama watu, hatuwezi kuwa na Dira ya Taifa inayoishia miaka 25 inayokuja. Hatuwezi kuwa wafupi hivi na kuruhusu uoni wetu uishie 2050. 

Nadhani swali la sisi tunataka kuwa taifa la aina gani, na lenye kuamini kwenye nini, linapaswa kuwa ni swali linaloangalia mbali zaidi, miaka 100 au zaidi mbeleni, huku majibu yake yakizingatia maslahi ya vizazi vya sasa na yale ya vinavyokuja.

Lakini hayo ni maoni yangu, na sasa Tanzania tuna Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Pamoja na mambo mengine, Dira inalenga kuibadilisha Tanzania, ndani ya miaka 25 ijayo, kuwa taifa endelevu, jumuishi na lenye kujitegemea. 

Hata hivyo, wakati lengo la kujenga uchumi wa kati wa Dola za Kimarekani trilioni moja ni jambo la kupongezwa, uchambuzi wa haraka haraka wa nyaraka hii muhimu utakuonesha namna ambavyo watungaji wake walishindwa kuzingatia kabisa usawa wa kitabaka kati ya wenye mitaji na wafanyakazi.

Dira, kwa namna ilivyoandikwa, inatoa kipaumbele cha juu na kikubwa sana kwa maslahi ya wafanyabiashara na wawekezaji, huku haki, umuhimu na maslahi ya wafanyakazi – ambao ndiyo injini ya uchumi huu unaofikiriwa – yakiwa kwa kiwango kikubwa yamewekwa kando. 

Siyo kwamba wafanyakazi hawatajwi kwenye Dira, la hasha! Wanatajwa lakini kama nyenzo ya wenye mitaji kuweza kufanya biashara zao vizuri; wanatajwa kama moja wapo ya njia Serikali inaweza kufanikisha ujenzi wa uchumi huu wa Dola za Kimarekani trilioni moja.

SOMA ZAIDI: Kitendawili Utekelezaji Dira 2050: Rais Samia Atoa Wito Kuchapa Kazi na Kuacha Mazoea 

Mtazamo huu uliochukuliwa kwenye kuandika nyaraka hii, na kufikiria hatma ya taifa letu mpaka kufikia 2050, unatishia kukuza pengo lililopo kati ya walionacho na wasionacho, na hivyo hata kuhatarisha kukwama kwa lengo la dira yenyewe la kujenga maendeleo endelevu na jumuishi yatakayomnufaisha kila Mtanzania.

Maendeleo endelevu

Maana ni muhimu sana kukumbushana kwamba kiini cha maendeleo endelevu ni kuwepo kwa mgawanyo sawa wa faida zitokanazo na maendeleo hayo. 

Wakati ukuaji wa uchumi ni ishara moja wapo ya taifa kupiga hatua, historia imeonesha mara kwa mara kwamba pale ukuaji huu wa uchumi usipoambatana na uwiano sawia kati ya maslahi ya wenye mitaji na yale ya wafanyakazi, tunachoweza kutabiri ni kuongezeka kwa pengo la kipato kati ya walionacho na wasionacho.

Taifa ambalo utajiri wa kupindukia wa watu wachache unaishi sambamba na ufukara wa kupindukia wa watu walio wengi, kama inavyoonekana kwenye nchi mbalimbali duniani, hatuwezi kuliita taifa lenye kudhihirisha afya, au hata mwisho mwema. Hilo ni bomu ambalo linasubiri kulipuka.

Kitendo cha Dira kusisitiza kwenye ujenzi wa “mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji” na kukuza “sekta binafsi,” bila kuweka msisitizo kwenye kukuza na kulinda haki za wafanyakazi, na uwezo wao wa pamoja wa kupigania maslahi yao, kinaweka mazingira ya hatari na kujenga hofu kwamba lengo la kujenga maendeleo “jumuishi” na endelevu litafanikiwa kweli.

Hatutakosea kwamba, kama hali itaendelea hivyo, Dira hii inatishia kujenga jamii ambapo kikundi kidogo sana cha watu kitalimbikizia faida zitakazotokana na ukuaji huo wa uchumi unaotegemewa, huku wafanyakazi, ambao ndiyo wazalishaji wakuu wa huo utajri, wakiachwa nyuma wakipambana na mishahara na maslahi duni.

Uzoefu kwengineko

Swali linaloweza kuja ni kwamba je, inawezekana kujenga taifa linalokusudia kukuza uchumi wake na hapo hapo kuwapa wafanyakazi wa taifa hilo nafasi kubwa kwenye namna uchumi huo unavyojengwa? 

SOMA ZAIDI: Profesa Shivji: Dira ya Taifa Haina Muda Maalum.Tusikubali Kufanyiwa Majaribio

Au, kwa maneno mengine, tukiwapa wafanyakazi uwezo mkubwa wa kulinda na kupigania haki na maslahi yao, hiyo haitaathiri juhudi zetu za kuvutia wawekezaji na kukuza uchumi na biashara nchini?

Na jibu la swali hili ni kwamba unaweza kufanikisha vyote hivi kwa wakati mmoja, kwamba siyo suala la kuchagua lipi na kuacha lipi. Hili linadhihirika zaidi tukiangalia nchi na Nordic kama vile Sweden, Denmark, na Norway ambazo zinasifika duniani kwa kuwa na viwango vya juu vya maendeleo na uchumi shindani, wakati huohuo zikiwa na vyama imara vya wafanyakazi na aina nyingine nyingi za ulinzi wa maslahi ya wafanyakazi.

Ingawaje kunaweza kuwa na sababu nyingi zinazoweza kuelezea mafanikio ya nchi hizi, ni maoni yangu kwamba hatuwezi kuacha kuyahusisha mafanikio hayo na mfumo zinaotumia ambao hutoa kipaumbele kwa mazungumzo na mashirikiano ya pande tatu kati ya Serikali, vyama vya waajiri, na vyama huru vya wafanyakazi kwenye kuhakikisha maslahi ya kila mmoja yanalindwa, na siyo mmoja ananufaika kwa gharama ya mwingine.

Utaratibu huu unahakikisha kwamba jitihada za ukuzaji wa uchumi zinakuwa ni mradi wa pamoja, ambapo wafanyakazi wana uwezo wa kutosha wa kushawishi aina ya mishahara na maslahi mengine wanapata, mazingira yao ya kufanya kazi, na mgao wa haki wa faida wanazosaidia kuzalisha. 

Hii siyo tu imesaidia kuzuia kukuza pengo la kipato kwenye nchi hizo, ikilinganishwa na nchi zingine zenye uchumi wenye saizi moja na wao, lakini pia imesaidia kukuza utengamano wa kijamii, uimara, na ukuaji wa uchumi wa muda mrefu. 

Mfano huu kutoka nchi na Nordic unathibitisha kwamba siyo tu kwamba inawezekana, lakini pia ni kwa manufaa ya taifa kwa sera na sheria kutungwa kwa kuweka uwiano sawia kati ya kukuza biashara na kulinda maslahi ya wafanyakazi.

Uwezo duni 

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hata hivyo, ni mwendelezo tu wa jitihada nyingi na muda mrefu za Serikali za awamu mbalimbali nchini Tanzania zilizolenga kudhoofisha uwezo wa wafanyakazi kupigania maslahi bora na mgao wa haki kwenye utajiri wanaozalisha kila siku.

SOMA ZAIDI: Tanzania Inahitaji Dira Moja ya Taifa, Ilani Tofauti za Vyama vya Siasa

Sera na sheria zinazoongoza masuala ya kazi nchini, wakati zikitoa ulinzi wa aina fulani kwa wafanyakazi, kwa kiwango kikubwa zinaweka vizuizi kwa wafanyakazi kuunganisha nguvu zao na kuweza kupigania maslahi yao kwa pamoja. 

Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, kwa mfano, inaweka utaratibu mgumu na mrefu ambao wafanyakazi wanapaswa kuufuata pale wanapotaka kuendesha mgomo halali, ambayo ni haki yao ya kisheria, hali inayoifanya migomo hiyo kushindikana kuratibiwa kabisa nchini.

Utaratibu wa utoaji taarifa na usuluhishi uliowekwa na sheria hii pia ni mrefu sana kiasi ya kwamba hata pale mgomo unapofanikiwa kuratibiwa malalamiko ya msingi yanaweza kuwa tayari yamepoteza uharaka wake, au utayari na ujasiri wa wafanyakazi kuyapigania unaweza kuwa tayari umeshapotea. Hii yote inawakosesha nguvu wafanyakazi, na kuweka mazingira ambayo yanawapendelea zaidi waajiri.

Mbali na sheria, uhusiano wa karibu pia kati ya vyama vya wafanyakazi na chama tawala, ambao ni wa muda mrefu, umevikosesha uhuru vyama hivi na uwezo wake wa kusimamia maslahi ya wafanyakazi, hususan pale maslahi hayo yanapokinzana na yale ya Serikali, au washirika wa karibu wa chama na Serikali.

Pale ambapo viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanapoonekana kuwa karibu sana na Serikali au waajiri, uwezo wao wa kupigania maslahi ya wanachama wao unapungua, na hivyo kuendelea kuwafanya wafanyakazi washindwe kufaidi jasho lao kama inavyopasa. 

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kushindwa kutambua madhaifu haya, na kwa kushindwa kupendekeza hatua madhubuti ya kuwawezesha wafanyakazi na vyama vyao, inakubaliana kwa namna fulani na hali kama ilivyo hivi sasa, na hata kutamani iendelee kuwepo. 

Marekebisho

Kwa hiyo, ili Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iwe kweli ni dira ya watu, ni lazima itekelezwe kwa namna ambayo itazingatia pia maslahi ya wafanyakazi. Hii inaweza kufanikishwa kwa Serikali kuchukua hatua kadhaa, ikiwemo kuzipitia upya sheria za kazi na kuondoa ukiritimba unaowazuia wafanyakazi kuunganisha nguvu zao kwenye kulinda na kutetea maslahi yao.

SOMA ZAIDI: Haya Ndiyo Yaliyofanya Dira ya Taifa ya 2025 Isifanikiwe Kikamilifu. Mchakato wa Dira ya 2050 Waanza

Ni muhimu pia Serikali na chama tawala zipunguze udhibiti na ushawishi wao kwa vyama rasmi vya wafanyakazi nchini ili wafanyakazi wawe na majukwaa yanayopigania kweli haki na maslahi yao badala ya kuwa na vikaragosi, taasisi zinazoonekana kama vyama vya wafanyakazi, lakini zinazojishughulisha na kukidhi matakwa na maslahi ya wafanyakazi.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni muhimu kwani inaonesha ni wapi Serikali inataka kuipeleka nchi kwenye miaka 25 inayokuja. Hata hivyo, uandishi wake, kwa kuyapa mgongo maslahi na mchango wa wafanyakazi, ikitoa kipaumbele kikubwa kwa wenye mitaji, ni tatizo ambalo hatuna budi kutafuta namna ya kukabiliana nalo ili kupunguza athari zinazoweza kutokana nalo.

Tutakuwa tunajidanganya kwa kuamini kwamba tunaweza kupima maendeleo ya nchi kwa kigezo cha GDP tu. Lazima maendeleo ya nchi yapimwe kwa kuangalia ustawi wa watu wake pia. 

Kwa kujifunza kutoka kwenye nchi zilizofanikiwa kuweka mizania kati ya maslahi ya wenye mitaji na wafanyakazi, na kwa kuchukua hatua madhubuti za kuwawezesha wafanyakazi wetu na vyama vyao, tunaweza kuwa na uhakika kwamba safari yetu kuelekea 2050 kweli ni ile yenye maendeleo jumuishi, na siyo yenye kukuza pengo kati ya walionacho na wasionacho.

Serikali ina wajibu mkubwa wa kuweka mazingira sawa yatakayoshawishi ukuaji wa biashara na uchumi nchini. Lakini ni ukweli pia kwamba Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kwamba ukuaji huo hautokei katika namna inayoathiri maslahi ya watu walewale ambao nguvu na jasho lao ndiyo zinategemewa kujenga nchi.

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×