Dar es Salaam. Ni ngumu kuhesabu mara ambazo Serikali imelazimika kutengeua uamuzi fulani saa chache tu baada ya kutangazwa, au kutoa ufafanuzi kuhusu hatua fulani iliyoichukua awali, kufuatia ukinzani mkali kutoka kwa wananchi walio kwenye mitandao ya kijamii, hususan mtandao wa Twitter.
Kwa miaka ya hivi karibuni, mtandao wa Twitter unaweza kusema umechukua nafasi iliyokuwa imeachwa na maandamano ya barabarani katika kupaza sauti za wananchi juu ya mambo mbalimbali ya kitaifa kiasi ya kwamba imekuwa ngumu kwa wale waliopewa dhamana ya uongozi wa nchi kupuuza kinachoibuliwa kwenye jukwaa hilo.
Ni katika muktadha huu ndipo wafuatiliaji wengi wa masuala ya Tanzania hawakushangaa pale Rais Samia Suluhu Hassan alipojitokeza hadharani na kutambua uwepo wa kile kinachojulikana kama Twitter Republic, au Jamhuri ya Twitter, jina ambalo wananchi watumiao mtandao huo, hususan wale wanaosimamia masuala ya kiutawala, wamejipatia.
Samia alikuwa akizungumza na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 17, Serengeti Girls, hapo Julai 5, 2022, kwenye hafla ya kuipongeza timu hiyo kwa kufuzu kwenda kwenye Kombe la Dunia baada ya kuifunga timu ya wanawake ya Cameroon.
“Huko kwenye mitandao kuna Jamhuri ya Twitter,” alisema Rais Samia wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam. “Sasa na sisi huku kwenye michezo tujenge Jamhuri ya Wapambanaji.”
Dk Aikande Kwayu siyo tu ni raia wa Jamhuri ya Twitter lakini pia ametumia muda wake kutafiti matumizi ya mtandao huo miongoni mwa vyama vya siasa vya upinzani ambaye ameiambia The Chanzo kwamba kukiri huko kwa Rais Samia juu ya uwepo wa Jamhuri ya Twitter kunatokana na kutambua kwake nguvu ambayo ‘Jamhuri’ hiyo inayo.
“Ni kwa sababu anajua ni kwa namna gani Twitter imekuwa ikichangia kwenye mijadala yenye kuleta chachu kwenye jamii na inawasaidia watu wengi,” alisema Dk Kwayu kwenye mahojiano hayo. “Mitandao ya kijamii, hususan Twitter, imesaidia sana wananchi kuweza kuongea na kutoa maoni yao na kuwafikia na kuwawajibisha viongozi wao.”
Kutingishwa kwa Jamhuri ya Muungano
Mifano ya namna Jamhuri ya Twitter ilivyowahi kuitingisha Jamhuri ya Muungano ni mengi sana kiasi ya kujaza kitabu. Mfano wa hivi karibuni kabisa ni uamuzi wa Serikali kuanzisha tozo kwenye miamala ya simu, uamuzi ambao unaendelea kupingwa vikali na wananchi waliowengi.
Na wakati ni ngumu kuhitimisha moja kwa moja kwamba hatua ya Serikali ya kupunguza, kwa mara mbili tofauti, viwango vya tozo hiyo, haitakuwa sahihi pia kutokutambua mchango uliotolewa na watumiaji wa mtandao wa Twitter kwenye kufanikisha hatua hiyo.
Hata Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, wakati akizungumza kwenye mkutano wa pamoja na mawaziri wengine na waandishi wa habari, hapo Septemba 1, 2022, uliolenga kutoa ufafanuzi juu ya tozo hizo, aligusia ukosoaji anaopata kutoka mitandaoni.
Vilevile, hatua ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kusitisha utaratibu mpya wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), siku tatu baada ya utekelezaji wake kuanza, inaweza kuhusishwa na ukinzani ambao utaratibu huo uliolenga kumzuia mteja wa NHIF kutibiwa kwenye hospitali nyengine mpaka apate kibali kutoka kwenye mfuko ulipata kutoka Twitter.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Wanasiasa Wanawake Wanaikimbia Mitandao ya Kijamii?
Kukiri kwa Rais Samia juu ya uwepo wa Jamhuri ya Twitter, hata hivyo, haimaanishi kwamba viongozi waandamizi wa Serikali wamekuwa wakifurahishwa na jukwaa hilo na mchango wake kwenye masuala ya kiutawala wa nchi. Mara kadhaa viongozi wamekuwa wakisikika kulalamikia mitandao.
Pengine moja kati ya kauli mashuhuri kuwahi kutolewa, kwa mfano, na Rais wa awamu ya tano Hayati John Magufuli ni ile iliyohusu kukerwa kwake na mitandao ya kijamii, akisema: “Natamani siku moja malaika washuke waizime hii mitandao [ya kijamii] yote.”
Hii ilikuwa ni mwaka 2017 na mpaka mwaka 2020 malaika hawakuwa wameshuka kuzima mitandao hiyo. Serikali ilifanya kazi hiyo. Kwa mara ya kwanza kwenye historia ya Tanzania, Serikali ilizima mitandao ya kijamii kwa takriban wiki kadhaa kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020.
Na hata baada ya mitandao mengine kufunguliwa, Twitter iliendelea kuwa haipatikani nchini Tanzania, hali iliyowapelekea wengi kutumia teknolojia ya VPN kuweza kutumia mtandao huo.
Rais Samia mwenyewe siyo mgeni kwenye kutoa matamshi yanayoonesha kutokukubaliana kwake na kile kinachofanyika kwenye mitandao ya kijamii. Mnamo Aprili 2021, kwa mfano, takriban mwezi mmoja tangu achukue hatamu za uongozi wa nchi, Samia aliishutumu mitandao ya kijamii kwa “uzandiki mkubwa.”
“Ukiingia kwenye mitandao ya kijamii kuna uzandiki mkubwa sana,” alisema Rais Samia aliyeapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania hapo Machi 19, 2021, baada ya kifo cha hayati John Magufuli. “Kila mtu anazua lake. Kila analofikiri kichwani kwake anaweka kule.”
SOMA ZAIDI: Kilichojificha Nyuma ya Kuvuja kwa Video za Utupu Mitandaoni
Kiota cha mijadala
Martin Maranja Masese ni mwanachama wa chama cha upinzani cha CHADEMA ambaye amejizolea wafuasi wengi kutokana na maoni yake anayochapisha Twitter kuhusu siasa na masuala ya utawala nchini Tanzania.
Masese anaisihi Serikali iache dhamira yake yoyote ambayo inaweza kuwa nayo ya kupambana na Twitter, akiuita mtandao huo “kiota cha mijadala ya kitaifa,” na kwamba kitu pekee Serikali inaweza kufanya ni kufuatilia na kutekeleza kinachojadiliwa huko.
“Twitter ni jukwaa kubwa sana,” alisema Masese wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Ni jukwaa ambalo limechukua nafasi kubwa sana kwa sisi Watanzania kuweza kusema kwa sauti zetu na kufikisha taarifa zetu kwa haraka kwa umma na Serikali.”
“Mijadala mikubwa inajadiliwa pale [Twitter] na taarifa zinafika kwa haraka kwa umma,” aliongeza mwanasiasa huyo na mwanaharakati. “Na kutokea Twitter imekuwa kama kiota cha [mijadala] kwenda kwenye mitandao mingine kama Whatsapp, Facebook na Instagram.”
Mtazamo wa Masese kuhusu Twitter kuwa “kiota cha mjadala” unaweza kuwa ni wa kweli kwani hata watumiaji wa WhatsApp, Facebook na Instagram, husambaza maoni ambayo huwa tayari yameshachapishwa kwenye mtandao wa Twitter.
SOMA ZAIDI: Anatumia Mitandao ya Kijamii Kuwatafutia Wenza Watu Wanaoishi na VVU
Ni ngumu kupata takwimu rasmi za utumiaji wa mitandao ya kijamii miongoni mwa Watanzania. Takwimu zilizopo, hata hivyo, zinaonesha kwamba Twitter ina watumiaji wachache sana Tanzania ukilinganisha na mitandao mengine ya kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa za Datareportal, mtandao unaotoa taarifa kuhusu shughuli za watu mitandaoni, mpaka kufikia Januari 2022, Tanzania ilikuwa na jumla ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wapatao milioni 6.1.
Kati yao, ni watu 470,000 tu, sawa na asilimia 1.2, ndiyo wanaotumia mtandao wa Twitter. Kwa mitandao mengine ni kama ifuatavyo: Facebook (milioni 4.3); Instagram (milioni 3.1); Facebook Messenger (milioni 1.1) na LinkedIn (laki tisa).
Uhuru wa kujieleza
Kennedy Mmari ni Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Bytes, kampuni inayotoa huduma za ushauri kwenye maeneo ya mawasiliano kwa umma, masoko na teknolojia, anayehusisha kuibuka kwa Jamhuri ya Twitter na uhuru ambao mtandao wa Twitter umekuwa ukitoa kwa wananchi kwenye kueleza mawazo yao.
“[Twitter] inaondoa hali ya kuzuiwa kwa mawazo,” alisema Mmari ambaye pia ni mtumiaji mzuri wa mtandao huo. “[Twitter] inatoa huo uhuru wa watu kujieleza bila kuhofia kwamba mawazo yao yatazuiliwa kufika pale yanapotakiwa kufika.
“Ukienda kwenye vyombo vya habari vya kawaida wana sera ya masuala gani ambayo watu wanaweza kuyazungumza na yale wasiyoweza kuyazungumza. Wana miongozo na maslahi ambayo yanaweza yakaguswa endapo jambo fulani litasemwa.
Lakini vile vile [kuna] uwajibikaji mkubwa kwenye misingi ya kisheria iliyowekwa hapa Tanzania hasa kwenye sheria za vyombo vya habari.”
Licha ya kutambua mchango mkubwa wa Twitter katika eneo zima la wananchi kusimamia na kuwawajibisha viongozi wao nchini, Dk Kwayu anadhani kwamba ili kujenga jamii yenye uwajibikaji haitoshi mapambano kufanyika mitandaoni tu.
SOMA ZAIDI: Jinsi ‘Tweet’ ya Mkurugenzi wa Asas Diaries Ilivyozua Gumzo Mitandaoni
“[Twitter] imesaidia kwa namna fulani lakini sidhani kama viongozi wameogopa vya kutosha,” anasema Dk Kwayu. “Hii mitandao ya kijamii inatakiwa iwe kama chombo cha mawasiliano na sehemu ya kujipanga, lakini lazima watu wafanye kazi huku chini ili kuendelea kusukuma.”
Dk Kwayu anashauri kwamba juhudi za kuchochea uwajibikaji wa Serikali ni lazima ziendelee mashinani, akionya kwamba kuna hatari kubwa sana kama vuguvugu linaendelea kubaki mitandaoni tu.
“Tanzania bado sana linapokuja suala la Serikali kuheshimu na kusikiliza wananchi wake,” alibainisha Dk Kwayu. “Na tukicheza, mitandao ya kijamii inaweza ikatudumaza kwa maoni yangu. Kwa hiyo, ni muhimu mapambano yakaendelea kwenye nyanja zote, mitandaoni na nje ya mitandao.”
Katuni kwa hisani ya Masoud Kipanya.
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.