The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Uchaguzi Mkuu Uganda 2026: Yanayofaa na Yasiyofaa Kuigwa Afrika Mashariki

Uchaguzi wa Uganda 2026 umekuja na matukio na vioja kadha wa kadha ambavyo ni ishara mbaya kwa demokrasia ya uchaguzi, visivyopaswa kuigwa

subscribe to our newsletter!

Nilitembelea Uganda kwa kazi maalum katika miezi michache iliyopita na kubaini kuwa joto la Uchaguzi Mkuu wa Uganda 2026 lilikuwa limepamba moto. Katika kipindi tangu wakati huo hadi leo, kumetokea mambo kadhaa ambayo yanafanya uchaguzi wa Uganda usiwe wa kuigwa katika ukanda wa Maziwa Makuu, Afrika Mashariki na Tanzania kipekee. 

Imienipasa kuandika makala hii kuyajadili mambo hayo, japo kwa uchache, kama sehemu ya kutahadharisha umma ili isionekane kana kwamba ni mambo ambayo yanaweza kuigwa na kuyaleta huku kwetu.

Kwa mujibu wa mfumo wa uchaguzi, Rais anachaguliwa na wapiga kura wote walioandikishwa kutoka miongoni mwa wagombea raia wa Uganda, wanaopaswa kuwa wametimiza umri usiopungua miaka 35 na ambao wana elimu ya angalau Kidato cha Sita. 

Ili kutangazwa kuwa amechaguliwa, mgombea lazima apate angalau asilimia 50 ya kura zote halali zilizopigwa. Katika mazingira ambapo hakuna aliyefikisha nusu ya kura zote halali zilizopigwa, duru ya pili hulazimika kuhusisha wagombea wawili vinara katika kinyang’anyiro hicho. 

Kwa uchaguzi wa wiki hii, watazamaji wengi wanabashiri kuwa kunaweza kuwa na ulazima wa mgombea wa Chama cha NRM, Rais Yoweri Kaguta Museveni na nyota wa muziki wa POP ambaye ni mgombea wa Chama cha NUP, Robert Kyagulanyi, ama Bobi Wine, kama ajulikanavyo mtaani. 

Katika ngazi ya Ubunge, Waganda wiki hii wanachagua jumla ya wabunge 529 kwa utaratibu ulio katika mafungu matatu: Wabunge 353 wa kuchaguliwa kupitia majimbo ya kijiografia; wabunge 146 wanawake watakaochaguliwa katika fungu la viti maalum vya wanawake; na wabunge wengine 30 watakaochaguliwa kujaza viti vya uwakilishi wa makundi mbalimbali ya Jamii ya Uganda kwa mujibu wa Sheria – Wanajeshi (10), vijana (5), wazee (5), wafanyakazi (5) na watu wenye ulemavu (5). 

SOMA ZAIDI: Uchaguzi Tanzania 2024 Na 2025: Tuna Nini Cha Kujifunza Kwa Majirani? 

Makundi haya yote yanachagua wawakilishi pasipo kujali itikadi za vyama vya siasa. Kwa makundi yote hayo, ipo lazima ya kuchagua angalau mwanamke mmoja kwa kila kundi na angalau wanawake wawili kwa kundi la wanajeshi wa UPDF kuingia Bungeni kwa sababu za kihistoria. Ili kuweza kukidhi sifa ya kuunda Serikali, chama cha siasa ni lazima kipate ushindi bungeni wa angalau viti 265 kati ya viti 353 vya uchaguzi majimboni.

Vitisho na utekaji

Katika mambo yasiyofaa kuigwa ni pamoja na vitisho na utekaji kwa wadau wa uchaguzi. 

Ni juzi tu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, Jaji Simon Byabakama Mugenyi, alijitokeza hadharani na kulalamika kuwa amepokea vitisho kutoka kwa baadhi ya watu wanaoamika kuwa karibu na mgombea wa chama tawala cha NRM, Museveni, kuwa asijaribu kumtangaza Mgombea wa NUP, Robert Kyagulanyi Ssentamu, hata kama atashinda uchaguzi kwa kuwa kufanya hivyo kutahatarisha maisha ya Mwenyekiti wa Tume. 

Hili linashabihiana sana na kauli ya msaidizi maalum wa Rais Museveni, Yiga Kisakyamukama, mwanzoni mwa wiki kuwa wapiga kura wanaaswa kurejea majumbani baada ya kupiga kura zao kwa vile mshindi wa uchaguzi ni Rais Museveni na si mtu mwingine yeyote, akisisitiza “Bobi Wine hata akishinda hatotangazwa.” 

Aidha, Rais Museveni mwenyewe amesikika akisema kuwa hata akishindwa uchaguzi hatoondoka Ikulu kwa vile Uganda ameitoa mbali sana, na kwamba “maendeleo yote yanayoonekana yasingepatikana” pasipo yeye. Kauli hizi zote ni mbaya kupitiliza katika nchi ambayo iko katika wiki ya uchaguzi wa Rais, wabunge na wawakilishi wengine wa serikali za mitaa.

Mbali na vitisho, Uganda imeshuhudia vitendo vilivyo kinyume na demokrasia ya uchaguzi katika kipindi cha ndani ya wiki moja iliyopita. Kwanza, kumekuwa na mashambulizi ya polisi dhidi ya wanasiasa wa upinzani. 

Katika wiki iliyotangulia tarehe ya upigaji kura, chama cha NUP kimelalamikia kutekwa au kukamatwa na polisi kwa kiongozi wa uhamasishaji na meneja wa kampeni wa chama hicho, Buwembo Habib, pamoja na viongozi na wanachama wengine wa chama kama Jamila wa Bobi, Zziwa Robert na Batabaale Ronald, ambaye pia ni mgombea. 

SOMA ZAIDI: Mambo Kumi Muhimu Kuboresha Muswada wa Tume ya Uchaguzi Tanzania

Wanne hawa walinyakuliwa wakiwa katika shughuli za kampeni barabara ya Masaka, wakijumuishwa na wapinzani wengi ambao wameshakamatwa na kuwekwa jela na kwingineko kizuizini, akiwemo Dr Kiiza Besigye wa chama cha FDC ambaye anashikiliwa tangu Novemba 2024 baada ya kunyakuliwa akiwa Nairobi nchini Kenya.

Mwezi Mei mwaka jana, mlinzi wa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Bobi Wine, aitwaye Edward Sebuufu, maarufu kama Eddie Mutwe, naye alipotea na baadaye kujulikana kuwa alikuwa ameshikiliwa katika ghorofa ya chini ya Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mwana wa Museveni. 

Tangia hapo, Eddie amekuwa akifikishwa mahakamani kwa tuhuma za ujambazi na unyang’anyi, lakini wakosoaji wanatuhumu kuwa hizo ni njama za kudhoofisha upinzani. 

Mapema mwezi Septemba 2025, naibu msemaji mkuu wa chama cha NUP,  Alex Waiswa Mufumbiro, alinyakuliwa na polisi kikatili nje ya mahakama jijini Kampala, akihudhuria usikilizaji wa kesi ya wanachama wengine wa NUP waliokuwa wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma mbalimbali ambazo NUP inadai ni za kubambikiwa. Hadi leo, Mufumbiro hajaachiwa huru, akiungana na orodha nyingine ndefu ya wapinzani wanaoshikiliwa kisiasa na Serikali ya Uganda.

Shambulio dhidi ya mashirika

Vitendo vingine vya hatari kwa demokrasia nchini Uganda vimekuwa ni pamoja na matishio na kufungiwa kwa mashirika makubwa ya kiraia na yale ya haki za binadamu nchini humo. 

Takribani wiki mbili zilizopita, Mkurugenzi wa Kituo cha Masuala ya Katiba (CCG), Dk Sarah Bireete, alifikishwa katika Mahakama ya Buganda kujibu tuhuma za kupatikana na taarifa za wapiga kura ambazo ni mali ya Tume ya Uchaguzi. 

Dk Bireete, ambaye ni mwanasheria mashuhuri na mtetezi wa haki za binadamu, alikamatwa nyumbani kwake wilayani Mukono mwishoni mwa mwaka jana na ataendelea kukaa rumande hadi baada ya Uchaguzi baada ya maombi yake ya dhamana kukataliwa na hakimu, licha ya kwamba hata upande wa mashitaka kutoweka pingamizi lolote. 

SOMA ZAIDI: Uchaguzi Umekuwa Kichocheo Kikubwa cha Marekebisho ya Katiba Tanzania 

Chama cha Mawakili nchini Uganda kimelaani vitendo dhidi ya Dk Bireete kwa kuviita “udhalimu na unyama wa hali ya juu.”

Wiki hii ya Uchaguzi, msajili wa asasi za kiraia nchini Uganda naye amekuja na jambo lake. Safari hii, mashirika saba makubwa yanayofuatilia uchaguzi na kutetea haki za binadamu na demokrasia nchini Uganda yamekumbwa na kadhia ya mrajisi. 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kampala, ofisi ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali imeyaandikia mashirika matano kuyaamuru kusitisha shughuli zao zote za miradi hadi hapo watakapotaarifiwa vinginevyo. 

Mashirika hayo ni pamoja na Chapter Four Uganda, Human Rights Network for Journalists – Uganda, Alliance for Election Finance Monitoring, the National NGO Forum, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu – Uganda, the Centre for Constitutional Governance kinachoongozwa na Dr Bireete, pamoja na African Center for Treatment and Rehabilitation of Torture Victims.

Katika barua zilizoyafikia mashirika hayo, ofisi ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali inadai kupokea taarifa za kiintelijensia zinazoonesha kuwa asasi hizo zinapanga kuhatarisha usalama wa Uganda, na kwamba ameelekeza taasisi hizo kusimamisha shughuli zake hadi uchunguzi wa mrajisi utakapokamilika. 

Mbaya zaidi, mrajisi huyo ameelekeza mabenki yote yanayotunza akaunti za fedha za asasi hizo kusimamisha utoaji wa fedha kwa wamiliki hadi mrajisi atakapoelekeza vinginevyo. 

SOMA ZAIDI: Mambo Muhimu Ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Tanzania 

Kwa maelekezo hayo, wafanyakazi wa taasisi hizo saba na familia zao hawatakunywa maji wala kula chakula hadi mrajisi atakapoamua kuruhusu malipo yao ya mshahara yalipwe na benki zao. Tabia hii ni ya kikatili na haifai kuvuka mipaka ya Uganda kwenda kokote kwingine kwa vile hata Uganda kwenyewe haifai.

Vitisho kwa wanahabari

Uchaguzi huu pia haujaiacha sekta ya habari na mawasiliano salama. Kumekuwepo na vitisho vingi kwa wanahabari na vyombo vyao vya habari, ikiwemo kutoka Tume ya Uchaguzi ya Uganda, ambayo kila mara imetishia wanahabari, au vyombo vitakavyojaribu kutangaza matokeo ya Uchaguzi. 

Aidha, kumekuwa na vitendo vya unyanyasaji wa waandishi unaofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama, huku Serikali kwa ujumla ikiwabana wanahabari katika ufanyaji wao kazi. 

Kwa mfano, katika miezi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu, wanahabari na vyombo vyao wamenyimwa taarifa muhimu na kusakamwa kwa utoaji wa taarifa za upotoshaji, jambo ambalo halipo kwa mujibu wa sheria kufuatia kufutwa kwa vifungu vya sheria kuhusu taarifa za upotoshaji kupitia mabadiliko ya Sheria ya Matumizi ya Komputa mwanzoni mwa mwaka 2023. 

Kuanzia wakati huo, hakuna tena kosa la jinai kwa sheria za Uganda linaloitwa “taarifa za upotoshaji” au fake news kwa kimombo.

Mamlaka ya Mawasiliano nayo imekuwa ikituhumiwa kutumika kisiasa kubinya uhuru wa habari na haki ya wananchi kupata taarifa. Kwa mfano, siku mbili tu zilizopita, Mamlaka ya Mawasiliano nchini Uganda (UCC) imeelekeza kuzimwa kwa huduma na mitambo yote ya kuwezesha intaneti hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Januari 15, 2026. 

Uamuzi wa UCC umewashangaza wengi ikizingatiwa kuwa mwanzoni mwa mwezi huu mamlaka hiyo hiyo ilitangaza kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu, Nyombi Thembo, kuwa Uganda isingezima intaneti wakati wa Uchaguzi wa 2026 kwa vile ilikuwa katika utekelezaji wa mkakati wa ujenzi wa uchumi shirikishi kupitia teknolojia. 

SOMA ZAIDI: ‘Kidole Kimoja Hakivunji Chawa’: Uchaguzi Mkuu wa Nigeria 2023 na Mambo Makuu ya Kujifunza Tanzania 

Imeshangaza dunia kuwa ndani ya wiki mbili, msimamo wa mamlaka umegeuka na kuzima mtandao nchi nzima na kuonya wale watakaobainika kutumia njia mbadala za kutumia intaneti kama vile kupitia teknolojia ya VPN.

Kwa ujumla, Uchaguzi wa Uganda 2026 umekuja na matukio na vioja kadha wa kadha ambavyo ni ishara mbaya kwa demokrasia ya uchaguzi, kiasi cha kutamani mambo hayo yaishie ziwa Victoria na yasije kuvuka na kuigwa na nchi majirani za Afrika Mashariki. 

Hizi ni nchi kama Kenya ambayo itakuwa na Uchaguzi Mkuu mwakani, 2027, au hata Tanzania ambako vuguvugu la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030 tayari limeanza mapema kwa ‘vikumbo’ vya hapa na pale vya wanasiasa wanaojiona wanatosha nafasi ya urais.

Mungu ibariki Afrika Mashariki!

Deus Kibamba ni mtafiti na mchambuzi anayefundisha Diplomasia na Sheria za Kimataifa katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dr Salim Ahmed Salim, Dar es Salaam. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.comkwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×