Dar es Salaam. Ukiwaona pamoja ni kama vile watu waliofahamiana maisha yao yote. Vicheko haviwaishi midomoni mwao, wakiteta hili na lile; Ida Hadjivayanis akimtambulisha kwa huyu na yule. “Huyu ni yule niliyekwambia,” au, “Huyu ni yule aliyekuandikia.”
Haichukui muda mrefu kuelewa kwa nini Ida ni mtu sahihi wa kutafsiri kazi ya Abdulrazak Gurnah, mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi 2021, kwa lugha ya Kiswahili, na tena tafsiri ya kwanza kwa lugha ya Kiafrika. Ida anasema hadharani kwa bashasha, “Mimi ni shabiki nambari moja wa Gurnah.”
Ni rahisi kudhani kwamba mapenzi yake Ida kwa Gurnah yanatokana na ushindi huo wa kimataifa alioupata mwanafasihi huyo. Lakini, sivyo. Ida alianza kumfuatilia Gurnah zamani kabla hajawa maarufu midomoni mwa Waswahili kama ilivyo sasa. Na hata huko Uingereza anakoishi, Gurnah hakufahamika sana kabla ya ushindi wake huo wa Nobel.
Ida anakumbuka jinsi alivyobeba kitabu cha Paradise, moja kati ya riwaya za Gurnah ambayo Ida ameitafsiri kama Peponi, na kukisoma kwenye fungate yake mwaka 2003 kwenye fukwe za Bara Hindi, akimwacha mumewe, Abshir Warsame, na kutokomea kwenye simulizi za Gurnah. Ilikuwa mara yake ya kwanza kumsoma Gurnah.
Ida alipomaliza kuisoma Paradise, alimwandikia Gurnah barua pepe mwaka uliofuata, akiendelea kufanya hivyo kwa kila kitabu cha mwandishi huyo alichokisoma. Na kila alipomwandikia, Gurnah alimjibu. Walitengeneza urafiki wa mwandishi na msomaji kwa jinsi hiyo.
Baadaye, Ida alianza kutumia vitabu vya Gurnah kufundishia, kikiwemo kitabu cha Paradise. Riwaya za Gurnah zilimpa Ida furaha alipozisoma kwani zilimwonesha ulimwengu ambao hakuuona sana kwenye kazi zingine za fasihi, mtafsiri huyo alieleza kwenye mahojiano aliyofanya nami hivi karibuni.
“Nilikuwa ninaona ulimwengu ambao sikuuona kwenye vitabu vingine vya simulizi za Kiafrika,” alinieleza Ida. “Ulimwengu ambao nimetokea mimi.”
Mwezi Oktoba mwaka 2023, ilikuwa mara ya kwanza kwa Profesa Gurnah na Dk Hadjivayanis kuwa nchini Tanzania kwa wakati mmoja kuchangamana na wasomaji pamoja na waandishi. Kila Gurnah alipoongea kwenye kadamnasi, macho yake Ida yalifunguka kwa mwangaza wa furaha na heshima. Mdomo wake uliopakwa rangi nyekundu ukifunguka kwa tabasamu kuonesha meno yake meupe yaliyojipanga vizuri.
Naye Ida alipozungumza, Gurnah, ambaye kichwa chake kimefunikwa na nywele nyeupe, alionekana kufuatilia maneno yake kwa umakini. Wakiwa pamoja, Ida hahitaji kutafsiriwa hulka na utashi wa Gurnah hata watu wengine wanapoonekana kujaribu kumdadisi kwa maswali yao mengi.
Mtu wa namna gani huyu? Mbona anazungumza na kuandika kwa Kiingereza? Anajua Kiswahili? Ni mwenzetu? Wao wanaelewana kwa vicheko na kusikilizana kwa adabu njema. Wakati mwingine, hata rangi za nguo zao zilishabihiana. Wawili hawa ni kama mtu na mwanae kiumri.
Mama yake Ida, Salha Hamdani, anasema alisoma wakati mmoja na Gurnah huko Unguja. Salha akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ben Bella na Gurnah Shule ya Wavulana King George V ambayo baadaye iliitwa Lumumba.
SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Hakuna Kiswahili Kimoja
Lakini ni dhahiri kuwa wanavyoheshimiana, ni zaidi ya suala la umri au asili. Ni heshima itokanayo na kuikubali kazi ya fasihi ambayo kila mmoja ameonesha kuwa nguli. Ida anasema ameona Gurnah anavyomheshimu kama mfasiri.
Walipofanya hafla ya kuweka sahihi zao kwenye vitabu huko Zanzibar, Gurnah alikataa kukaa kiti cha tofauti na Ida, akiomba wote waletewe viti vyenye urefu na muundo unaofanana, na tena vitazamane wakiwa wanaweka sahihi vitabu vya wasomaji mbalimbali waliofika hapo kwa ajili hiyo.
Mara ya kwanza kwa dunia kuwaona pamoja ilikuwa Oktoba 2022 kwenye uzinduzi wa kwanza wa kitabu cha Peponi uliofanyika kwenye Kongamano la Kiswahili la Baraza SOAS, Chuo Kikuu cha London. Ida ni Mhadhiri Mwandamizi wa Masomo ya Kiswahili katika chuo hicho wakati Gurnah ni Profesa wa Masomo ya Kiingereza na Fasihi za Kikoloni katika Chuo Kikuu cha Kent.
Mwaka mmoja baadaye, wawili hao walijilipia tiketi ya ndege na kusafiri mpaka Unguja kwa ajili ya kuhudhuria Tamasha la Vitabu la Zanzibar kwa mwaliko wa Ally Baharoon, mwandishi na mdau wa usomaji, aliyeliandaa tamasha hilo la kwanza visiwani humo kwa kushirikiana na wadau wengine likivutia zaidi ya watu 1,500.
“Tumerudisha kitabu nyumbani,” alisema Ida, akiongea kwenye tamasha hilo.
Paradise, iliyochapishwa mwaka 1994, ni moja ya riwaya kumi alizoandika Gurnah. Ni riwaya ya kihistoria inayoangazia maisha ya wana Afrika Mashariki mwanzoni mwa karne ya ishirini. Kijana mdogo Yusuf anawekwa rehani na babake kwa mfanyabiashara aliyejulikana kama Ami Aziz ili kulipa deni. Safari wanayoianza inaufungua ulimwengu mpya kabisa kwa kijana huyo, anakua na kubalehe, anaonja madhila ya ukoloni na mabaya mengine kwenye jamii ya wakati huo.
Wakiwa kwenye uzinduzi wa Peponi Zanzibar, na kisha Dar es Salaam, wazazi wake Ida wanaambatana naye. Wamekuwa wakimuunga mkono binti yao huyo wa kwanza pamoja na mdogo wake, Inessa, tangu wakiwa wadogo. Walikuwa wanavaa nyuso zilizojaa tabasamu na furaha wakati wote.
Safari ya mfasiri
“Niwe mkweli, sikuwahi kufikiria kuwa Ida atafika hapo alipofikia,” alinieleza Salha, mama yake Ida, kwa tabasamu kubwa tukiwa tumeketi nyumbani kwa dada yake, Zakia Meghji, jijini Dar es Salaam.
Salha, ambaye ni mwalimu kitaaluma, amefundisha masomo ya sayansi Shule ya Kilakala mkoani Morogoro kwa miaka mingi kabla ya kujiunga na shirika la Umoja wa Mataifa ambalo alilitumikia mpaka alipostaafu. Kama ilivyo kwa wazazi wengi wa Kiafrika, Salha alitamani watoto wake wawe na kazi zinazofahamika – mwalimu au daktari. Binti zake walipokuwa wadogo, alitamani wachukue mkondo wa sayansi.
“Nakumbuka tulikuwa tunaamka alfajiri, tunasoma Biolojia, Kemia, Hesabu – yote nimewasomesha binti zangu, nikiwaandaa kwa mitihani yao,” anasimulia. Japokuwa Ida aliyamudu masomo ya sayansi vizuri, aliamua kuwa anataka kufuata njia nyingine.
SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis Aichambua ‘Peponi’ Ya Abdulrazak Gurnah
“Aliposema anataka kusoma masomo ya lugha, niliwaza kuwa labda akimaliza atakuwa mwalimu wa chekechea au shule ya msingi,” Salha aliendelea kusimulia. “Lakini kama Waunguja wanavyosema, aliyepewa kapewa [na] wala hapokonyeki. Ninazidiwa na hali ya furaha nikiangalia hapa alipofikia. Mimi na baba yake tunaendelea kumwambia aendelee kuwa mnyenyekevu katika safari yake.”
Walipooana, Salha alikuwa na miaka 21 na George alikuwa na miaka 25. Mara tu baada ya kufunga ndoa, Salha alifundisha wanafunzi wa sekondari kama sehemu ya mafunzo ya jeshi, au national service kwa kimombo, kwa miaka miwili na kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikosomea masomo ya Botania na Zoolojia.
Ida akazaliwa jijini Dar es Salaam mwaka 1977 Salha alipokuwa na umri wa miaka 28, wakati huo walikuwa wakiishi Morogoro.
Alipokuwa na kama miaka miwili na nusu, bibi yake Ida mzaa mama aligundua kuwa kila mjukuu wake huyo alipopanda kilima kidogo karibu na kwao, alikuwa anahema sana. Akamwambia Salha, ambaye kwa wakati huo alikuwa mjamzito. Hazikupita siku nyingi, rafiki yao wa karibu ambaye alikuwa daktari alipita hapo nyumbani na kumkuta Ida akiwa anacheza.
Daktari huyo akamkagua Ida kwa utaalamu wake wa kidaktari na kumweleza George kuwa kulikuwa na tatizo. Siku si nyingi, wakafunga safari kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.
Ida akaonekana kuwa na ‘Patent ductus arteriosus’ (PDA) ambapo mshipa unaotoa damu kutoka kwenye moyo unakuwa haufungi. Binti mdogo Ida akapewa miezi sita tu ya kuishi. Daktari waliomwona wakasema kuwa wanaweza kumpa nafasi ya matibabu, au appointment, baada ya miaka sita.
Ukweli ni kwamba, kulikuwa hakuna vifaa vya kumfanyia Ida upasuaji. Wazazi wake walishikwa na wasiwasi, maana walikuwa hawana uwezo wa kumpeleka nje ya nchi kwa ajili ya matibabu na muda ulikuwa unawatupa mkono.
“Ndugu wakasema watachanga,” Salha anakumbuka. “Zakia akasema apelekwe Moshi ili tumpeleke Nairobi, maana yeye alikuwa anaishi Moshi wakati huo. Hatuwezi kuacha mtoto atufie mikononi. Kufika pale, kukawa na timu ya madaktari imekuja. Wakasema aje hapahapa, hamna haja ya kwenda Nairobi. Mambo yakapangwa, lakini kukawa na tatizo.”
“Wakasema madaktari muhimu hawawezi kuja,” aliendelea kusimulia Salha. “Wakaniambia upasuaji unaweza kuwa wenye mafanikio lakini wakati mwengine watoto hufa kwa kukosa matunzo mazuri baada ya upasuaji. Basi, ikashindikana, tukarudi nyumbani. Tukamshukuru Mungu, labda alituepusha. Maana hatujui baada ya kufanyika [upasuaji] ingekuwaje. Lakini Kenya tusingeweza kwenda, hatukuwa na kitu. Tulikuwa masikini tu.”
Ikatokea kama muujiza ambapo rafiki yao akina Salha, ambaye alikuwa amewahi kufundisha na George, aliwatembelea nyumbani kwao. Rune Skarstein na mkewe, ambaye na yeye pia aliitwa Ida, walipoelezwa juu ya uhitaji uliopo, wakawaambia waandae pasi ya kusafiria, huku Salha akiwa hana matumaini kwamba chochote kinaweza kufanyika.
SOMA ZAIDI: Tamasha la Vitabu Zanzibar: Kitovu cha Vipaji Vipya?
Cha kushangaza, hazikupita siku nyingi Skarstein akawaeleza kuwa amezungumza na marafiki zao wengine waliokuwa nchini Norway kutoka Tanzania, nchi tofauti za Kiafrika na Kiskandinavia nao waliamua kuanzisha “Ida Fund”. Ikabidi maandalizi yafanyike haraka, George akaenda na Ida kwani Salha alibaki na Inessa, kitoto kichanga.
Daktari bingwa ambaye walitaka afanye upasuaji alikuwa ndiyo tu amestaafu. Wakamsihi sana afanye upasuaji wake wa mwisho, akakubali. Siku ya upasuaji, wote walimficha Salha. Wakamwambia kuwa utafanyika kesho yake. Upasuaji ulipomalizika baada ya masaa saba, George alimpigia mkewe na kumpa habari.
“Aliniambia, mtoto amepona. Sikuweza kuamini,” anakumbuka Salha, sauti yake ikitetemeka. “Akaniambia, yeye mwenyewe alilia.” Salha alishindwa kujizuia, akayaachia machozi yatoke na kisha akakaa kimya kwa sekunde kadhaa akiitafakari kumbukumbu ile.
Fedha zilizobaki zilitumika kumsaidia mtoto mwengine aliyehitaji matibabu. Ida mwenyewe anasema kuwa, daima atawakumbuka watu wa Norway kwa kumpa nafasi nyingine ya kuishi. Mama yake anawaza, dunia ingekuaje kama Ida asingepona. “Mara nyingine huwa nafikiria, Ida asingekuweko,” Salha aliwaza. “Sijui labda tafsiri hii, sijui. Peponi, sijui.”
Masuala ya utambulisho
Gurnah aliposhinda Nobel, kulikuwa na majadiliano mengi ya hapa na pale. Je, yeye ni Mtanzania? Je, yeye ni Mzanzibari? Mtanzania ni nani? Mpaka leo anatambulishwa kama Muingereza mwenye asili ya Tanzania na wengine husema, mwenye asili ya Zanzibar. Ida hajakutana na tatizo hilo kwani yeye ni raia wa Tanzania japokuwa ameishi Uingereza muda mrefu. Hata hivyo, jina lake huibua maswali kwa anayelisikia kwa mara ya kwanza.
Hadjivayanis? Watu wa wapi hao? Kama ilivyo kawaida yetu kuuliza tukisikia jina la mtu.
Yeye mwenyewe Ida anasema hiyo haimsumbui. Anakumbuka akiwa shuleni watu walikuwa wakimwita majina kama mzungu, mzungu koko lakini hakuwekea maanani kwani aliona ni utani tu. Ni mpaka alipofika Uingereza, ndipo alipoanza kujiona kuwa ni wa tofauti.
“Kule [Uingereza], haraka sana wanataka ufahamu kuwa wewe siyo wa hapa – ni mhamiaji,” alinieleza Ida wakati wa mazungumzo yetu. “Na Gurnah anagusia mambo haya, akionesha kuwa yapo tangu zamani kwenye historia. Kwa mfano, Yusuf anatoka mji mmoja ambao nadhani upo maeneo ya Tanga, japokuwa simulizi hauutaji waziwazi, kisha anakwenda kwa Wamanyema. Anaonekana tofauti lakini yeye mwenyewe anajiona ni mtu wa hapohapo. Nami pia, nimejikubali kuwa mimi ni mtu wa hapa [Tanzania].”
Yeye na mumewe wanawalea watoto wao Aaliyah (18), Hannah (13), Mikhail (10) na Amin (4) katika misingi hiyohiyo – kujitambua kama Watanzania japokuwa wanaishi Uingereza.
Baba yake Ida, George Hadjivayanis, ni Mtanzania mwenye asili ya Ugiriki. Alizaliwa na kukulia Dodoma kabla ya kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye kufundisha Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro. Babu yake George alikuwa William Frech, Mjerumani aliyesimamia ujenzi wa reli ya kati kama mhandisi mkuu.
Frech alimwoa Tausi binti Abdallah na kupata watoto wawili, Otto na Ida. Binti yao Ida alikutana na Galinos Hadjivayanis kwenye stesheni ya reli Dodoma. Yeye alikuwa muuza bucha, Mgiriki aliyehamia Tanganyika akiwa kijana. Wakaoana, wakawa wazazi wa George.
SOMA ZAIDI: Ushindi wa Gurnah Uikumbushe Serikali Umuhimu wa Uraia Pacha
“Baba yake George alikuwa anauza bucha,” anakumbuka Salha. “Alikuwa ni Mgiriki wa kawaida. Aliugua, akazikwa hapahapa. Lakini watu wakisikia Mgiriki wanajua ana pesa,” aliongeza Salha, akicheka.
Wanawake waliomkuza
Ida alipokuwa mdogo, bibi yake mzaa mama, Salama binti Rubeya, alikuwa anamwita na kumtaka amsomee – kitabu, gazeti, kanga, chochote kile ilimradi amsomee kitu. Binti mdogo Ida alifurahia sana jambo hilo kwani alipewa pesa kidogo kama shukurani. Ikafika mahali, hakujali tena vijisenti, alisoma kwa mapenzi ya hadithi.
Kila siku, akawa anafanya mazoezi ya kusoma mpaka akawa anazijua hadithi zote kwa kichwa na kwenda kuwasimulia wenzake shuleni. Ikamjengea hamasa kubwa ya kupenda fasihi tangu alipokuwa mdogo.
Hata hivyo, yeye si mtafsiri wa kwanza kwenye familia yao. Mama yake ananisimulia kuwa baba yao alikuwa kadhi enzi za uhai wake. Tena alikuwa mtafsiri kortini, enzi za mkoloni.
“Baba yangu alifariki nikiwa na miaka miwili,” aliniambia Salha. “Yeye alikuwa mkalimani kortini enzi za mkoloni. Alitafsiri Kiswahili kwenda Kiingereza. Hata Kiarabu kwenda Kiingereza. Kihindi pia alikijua. Unajua zamani, watu walikuwa wanajua lugha zote za jamii zilizokuwepo. Mpaka Kijerumani, wakati ule.”
Mzee Mohammed Hamdani aliishi Kilwa japokuwa alitokea Unguja. Akina Hamdani ni wazaliwa wa Unguja kwa vizazi saba nyuma. Akiwa huko Kilwa, alimwoa Salama ambaye walipishana umri kwa zaidi ya miaka 30.
“Alipopeleka posa, mama aliuliza – anajua Kizungu? Anajua kusoma na kuandika?” anasema Salha, akitabasamu. “Akaambiwa eeh, anajua. Basi, hayo yalimtosha.”
Ida anatoka kwenye familia iliyokuwa na wanawake shupavu; wanawake walioshika nafasi kubwa za uongozi, na hata kuwa viongozi katika jamii zao. Mama yake anakumbuka malezi ya bibi yake yeye.
“Bibi yangu mimi, Zaidani binti Mbwana, alikuwa Mngindo – mama yake mama yangu,” Salha alinisimulia, huku akionekana kusisimka kwa simulizi yake mwenyewe. “Alikuwa anajivunia sana kuwa kabila lao ndiyo walipigana vita vya Maji Maji. Alikuwa Mngindo shupavu haswa. Ndiyo wote hawa kina Zakia unaona wamekuwa viongozi, ni kutokana na bibi yetu. Kila mara alikuwa ananiambia, usikubali kuonewa.”
Dada yake mwengine, Maryam Hamdani, ni mwanahabari na mwanaharakati maarufu anayeishi Zanzibar. Ni mwanzilishi wa kikundi cha kwanza cha wanawake wanaoimba Taarabu kinachoitwa Tausi. Salha anafafanua kuwa, nafasi ya bibi yake Ida kumjenga kifasihi ni kubwa mno. Japokuwa yeye na mumewe ni walimu, na yeye mwenyewe alijitahidi kumshawishi Ida kupenda masomo ya sayansi ambayo aliyamudu, bado aliamua kuchukua mkondo wa fasihi.
SOMA ZAIDI: Utafiti wa Kijenetiki Wabainisha Asili ya Waswahili wa Afrika Mashariki
Kielimu, Ida alisoma Shule ya Msingi Mlimani huko Morogoro, halafu akaenda Shule ya Sekondari Morogoro baba yake akiwa anafundisha Chuo Kikuu cha Sokoine na mama yake akiwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Kilakala.
Akahamia Dar es Salaam kwa ajili ya masomo yake ya ‘A-Level’ ambapo alisoma Shule ya Wasichana Zanaki akichukua Kiswahili, Literature na French (KLF). Huko Dar, alifikia kwa mama yake mkubwa, Zakia Meghji, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Muungano.
Salha anamshukuru sana dada yake kwani alimlea Ida kwa kipindi hicho. Baadaye Ida alisoma ahahada yake ya kwanza nchini Lesotho na kisha kwenda Uingereza kwa ajili ya Shahada yaUzamili na Shahada ya Uzamivu.
Waliishi Ufaransa kwa miaka miwili, George alipokuwa anasomea shahada ya uzamivu, Ida akiwa na umri wa miaka 10 hivi. Wakiwa huko, wakajifunza lugha ya Kifaransa ambayo waliendelea kuzungumza hata waliporudi Tanzania.
Ilikuwa ngumu kuwarudisha kwenye lugha ya Kiingereza na Kiswahili, lakini wazazi wao walikuwa makini kuhakikisha kuwa kila lugha ina mahali pake. Nyumbani, mama yao aliwaongelesha Kiswahili na Kiingereza. Baba yao, Kifaransa. Na tena Kifaransa kikawa lugha ya faragha kwa Ida na Inessa.
“Na hata sasa, Ida na Inessa wakitaka kuteta jambo, au kuongea kitu kizito, wanabadilisha lugha na kuanza kuongea Kifaransa,” mama yao anasema.
Kumtafsiri Gurnah
Wakiwa wanatembea Mji Mkongwe, Gurnah alikuwa akimuuliza Ida maana ya maneno mapya. “Kuna maneno mengi ya Kiswahili ambayo hayajui,” anasema Ida, akieleza kwamba Kiswahili cha sasa si kama kilichokuwa kinazungumzwa wakati wa ujana wa Gurnah alipokuwa akiishi Zanzibar.
Pamoja na kutafsiri kazi za Gurnah kwa ulimwengu, kwa namna fulani anautafsiri ulimwengu kwa Gurnah. Lakini Gurnah hana upungufu wa maneno. Ukikaa naye kwa dakika tano, utagundua kuwa haogopi kutamka maneno ‘makubwa makubwa’ ambayo kwa Kiswahili yanaweza kuwa makali masikioni mwa watu.
Hata katika uandishi wake, hana tafsida. Japokuwa kwake Ida kazi ya kutafsiri haikuwa ngumu sana, anakiri kuwa alikuwa na kazi kubwa ya kupunguza ukali wa maneno ambayo Gurnah ametumia kwenye Paradise.
Tukiwa tumekaa mezani nyumbani kwa Zakia, Salha alisema: “Na tena kuna maneno mengine, kwa mfano, kwa Kiingereza wanasema ku-sodomise. Ida ametumia neno la Kiunguja, kumkaza [ambapo Gurnah ametumia to screw]. Lakini [zamani] Unguja huwezi kusema kukaza.”
SOMA ZAIDI: Watanzania na Kilio cha Samaki Kwenye Maji Katika Kiswahili
Salha alikuwa akisema kwa sauti ndogo japokuwa hakuna mtu mwingine mezani zaidi yetu, na kuongeza: “[Ila] hiyo [kukaza] ni afadhali kuliko kumwingilia. Lakini lugha ya zamani ya Abdulrazak, na hata sisi tulipokuwa tunakuwa ni kumkaza.”
Kiswahili bado kina usiri. Kuna maneno ukiyataja, watu wanashtuka.
Ida anaeleza: “Unapotumia Kiingereza, ule utamaduni [wa lugha hiyo] umeshakubali maneno na matendo fulani. Hapa [Tanzania], bado hayajakubalika. Kwa hiyo, huwezi kusema kwamba kwa sababu ninatafsiri kazi ya Gurnah na yeye ni mwandishi wa kimataifa, basi nitatumia lugha kwa muktadha huo, hapana.”
Hamid: ‘… I feel sorry for you sometimes, Kalasinga, whenever I think of your hairy arse sizzling in hell-fire after the judgement day,’ and Kalasinga replies, ‘I’ll be in paradise screwing everything in sight. Allah Wallah, while your desert God is torturing you for all your sins.’ Kalasinga replied cheerfully. (Gurnah, Paradise, p. 102).
Hamid: “… Ninakuhurumia mara nyingine, Kalasinga, kila wakati nikifikiria utupu wako wa nyuma uliojaa nywele ukichachatika katika moto wa jahanam siku ya kiama.’ … ‘Mimi nitakuwa peponi nikikaza kila kitakachoweza kukazika mbele yangu, Allah-wallah, wakati Mola wenu wa jangwani akiwatesa kwa madhambi yenu,’ Kalasinga alijibu kwa uchangamfu. (Hadjivayanis, Peponi, uk. 104).
Katika tafsiri ya awali ya ubishi wa kidini kati ya Kalasinga, ambaye anatoka India, na Hamid, ambaye ni Mswahili na Muislamu, Ida alitumia neno mavuzi kama tafsiri ya hairy arse. Lakini baada ya kushauriana na mchapishaji, waliamua iwe nywele.
“Kulikuwa na mapumbu pia,” anasema Mkuki Bgoya, Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuki na Nyota, wachapishaji wa Peponi, kwa kicheko.
Bgoya anakiri kuwa baada ya kuona kuwa kuna baadhi ya maneno ambayo ni makali kwa Kiswahili, ilibidi wayajadili.
“Kazi yetu [wachapishaji], si kumfunga mdomo mwandishi au mfasiri,” anafafanua Bgoya. “Ni kweli tuna maslahi yetu. Lakini ilimradi kubadili kitu hakutaidogosha maana, tutajaribu kushawishi maneno, au tafsiri, mbadala. Kama itaeleweka, ni sawa, ili tufikie kila mahali, ikiwemo shuleni.”
Kwa bahati nzuri, Ida alikuwa na mawazo yanayofanana. Lengo ni watu wengi wamsome Gurnah. Lakini sasa anafikiria kutoa toleo lingine ambalo halitaondoa ukali wa maneno na kuakisi lugha aliyotumia Gurnah, ambacho hakitatumika shuleni.
Mama yake alikuwa na maoni tofauti kuhusu matumizi ya maneno ambayo bado hayajashibwa na jamii.
SOMA ZAIDI: Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu: Tumaini Jipya Kwa Waandishi Tanzania?
“Achana na shuleni, hata watu wazima hawatasoma,” Salha alimtahadharisha Ida, huku Ida mwenyewe akicheka. “Wewe mwenyewe umesema ulikuwa unamsomea bibi yako ukiwa mdogo. Na angekuwa hai pengine ungemsomea bibi yako. We ungemsomea bibi yako [maneno hayo], na angesema: ‘laana, laana tupu.’”
“Jamii bado haiko tayari,” Salha alihitimisha hekima zake.
Esther Karin Mngodo ni mwandishi, mshairi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa.
One Response
Maelezo yakina ningefurahi walau haya yakaingizwa katika Gazeti la Zanzibar la Kila Siku, ”Zanzibar Leo” katika uwono wangu juu ya Wazanzibari hawa wawili na kazi kubwa wanaoifanya katika FASIHI kujulikana kwao bado hakujafikia kuwtanbulikana kunavyostahiki.
Nimeona kwenye Tamasha la Vitabu waliokuwepo ni wengi ni katika Duru ya wana taaluma wakati usomaji wa vitabu hauna mipaka, watu wa kawaida nao husoma vitabu na kuvifaidia.
Wakati hapa nyumbani kuanzishwa Elimu ya Watu Wazima kuna mzee tukiishi naye ambaye alipigana vita vya pili vya Dunia kisha akawa baharia, bahati mbaya mzee huyu hakujua kusoma na kuandika akajiunga katika Elimu ya Watu Wazima bara Ikitwa Elimu ya NGUMBARU, nikiwa nipo Std V kati waliokuwa wanamsaidia kusoma na akipenda kusoma gazeti la Uhuru baada ya kujuwa kusoma na akishalinunua gazeti kitu cha kwanza hymsoma CHAKUBANGA na akiweza kuwaelezea kwa siku ile Chakubanga kafanya nini na hero wake alikuwa Bushiri. Baadayae mzee huyu alianza kununua vitabu vya Abunuwasi, Esspo, Mashimo ya Mfalme Sleiman, Kisiwa cha Hazina na vyenginevyo tukastaajabu kasi aliokuwa nayo yakusoma.
Tulikuja kujuwa yule mzee alikosa fursa ya kupelekwa Skuli na wazee wake lakini akili yake ilikuwa Sumaku.
Nakumbuka namna alivyokuwa akikielezea Kitabu cha Kusadikika akisema huyu Shaabani Robert katokea wapi?
Ninachokieleza hapa nikuwa hata watu wa kawaida husoma vitabu, kwahio Lulu hizi mbili bado kunakazi yakuwajulisha katika eneo laasili yao.